Sisi ni LEO na KESHO ya TANZANIA

Written by Eberhard Osward | Posted on  19 Feb 2016.


Kuna wakati najaribu kuwatazama na kujifunza vitu mbalimbali kutoka kwa wadudu, wanyama na hata mimea. Moja kati ya wadudu wanaonivutia sana ni mchwa. Mchwa ni wadudu wadogo sana lakini ni wadudu ambao achilia mbali udogo wao, wamekuwa ni wajenzi wakubwa sana wa vichuguu ambavyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikitumiwa na wadudu wengine na wakati mwingine hata wanyama kama sehemu ya makazi. Baada ya kujifunza kwa muda mrefu kutoka kwa mchwa, nimekuja kugundua na kujifunza vitu vikubwa vitatu ambavyo vinawafanya mchwa kuweza kufanikisha kujenga vichuguu vikubwa achilia mbali udogo walio nao, vitu hivyo ni UMOJA, UPENDO na USHIRIKIANO.

Nimejaribu kuelezea historia fupi ya mchwa kwa dhumuni la kuonesha nguvu ya Umoja, Nguvu ya Upendo na Nguvu ya Ushirikiano. Ili tuweze kupiga hatua kama taifa na kuweza kuijenga nchi yetu ni dhahiri kwamba tunatakiwa kuwa na umoja, upendo na ushirikiano baina yetu. Hata kama Rais wetu Mh. John Pombe Magufuli akiwa rais mzuri kiasi gani, kama sisi vijana, kama sisi wananchi hatuna umoja hatuwezi kufanikiwa kwenye kazi zetu binafsi na hata katika jitihada zetu za kulijenga taifa hili, kwa sababu achilia mbali kwamba umoja ni nguvu ila pia umoja unaleta uwajibikaji, pia kukiwa na umoja baina yetu ni rahisi sana kwa serikali kutusaidia wananchi wake kwenye vikundi kuliko kumsaidia mtu mmoja mmoja,vivyo hivyo hata kama Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa akifanya juhudi kiasi gani hatuwezi kupiga hatua kwenye nyanja zote za maisha kama vile kiuchumi, kisiasa na hata kijamii kama hakutokuwa na ushirikiano mzuri kati ya wananchi na serikali kwani endapo tutashirikiana kwa ukaribu na serikali yetu ni dhahiri kwamba serikali itajua matatizo yetu na pia wananchi tutakuwa na nguvu na uwezo wa kuiwajibisha serikali pale itakapokosea sababu serikali ni sisi.

Nguzo kubwa itakayotufanikisha kuleta umoja na ushirikiano ni UPENDO, sio tu upendo baina yetu sisi, bali upendo kwa taifa letu na hata kwa vizazi vijavyo. Tukiwa na upendo, hatutojali matumbo yetu tu, tutawakumbuka na masikini walio vijijijni, tukiwa na upendo hatutowaza kujilimbikizia mali, tutawakumbuka na walemavu wanaoshindwa kupata huduma za kijamii, tukiwa na upendo tutatumia rasilimali katika njia bora itakayofanya vizazi vijavyo kufurahia matunda ya matumizi bora ya rasilimali hizi na kuleta maendeleo endelevu.