IMETOSHA SASA!!

Written by Eberhard Osward | Posted on  26th Feb 2016.Kwa muda mrefu sana sanaa ya Tanzania imekuwa ikifanywa kama shughuli fulani inayofanywa baada ya muda wa kazi na sio shughuli rasmi ya kiuchumi. Kwa muda wote huo wasanii wamekuwa wakilalamika kuwa wanaibiwa kazi zao, wasanii wamekuwa wakilalamika kuwa hawanufaiki na kazi zao sababu kubwa ikiwa ni kwamba kazi zao zimekuwa zikitumika bila wao kunufaika na wakati mwingine zimekuwa zikirudufishwa (Piracy) na hivyo kupata hasara. Leo ningependa kuzungumzia hakimiliki za kazi za sanaa na pia ningependa kuwakumbusha wasanii juu ya haki ya kumiliki mali kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Sehemu ya Tatu kifungu cha 24 (i) na (ii), katiba inaelezea haki ya kumiliki mali na pia haki ya kulindwa kwa mali za raia yeyote. Nitaanza kwa kunukuu kifungu cha 24 (i) na kuelezea kidogo juu ya haki ya kila raia ya kumiliki mali, kifungu hicho kinasema

“ 24.(1) Bila ya kuathiri masharti ya sheria za nchi zinazohusika, kila mtu anayo haki ya kumiliki mali, na haki ya hifadhi kwa mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria.” Kifungu hiki kinampa kila mwananchi haki ya kumiliki mali na pia haki ya mali yake kuhifadhiwa. Hiyo basi kazi yako ya sanaa, iwe muziki, mashairi, kazi ya uchoraji, uchongaji, ubunifu wa mavazi, uigizaji na kazi yako yoyote ya sanaa ni mali yako. Kisheria neno mali linamaanisha vitu vinavyotawaliwa na mtu kama vyake, hivyo basi wewe kama msanii, kazi yoyote ambayo umeitengengeneza na kuiandaa kwa kutumia nguvu na akili yako hiyo ni mali yako, una haki ya kuimiliki. Ila kumbuka na zingatia kitu kimoja, ili mtu aweze kumiliki nyumba, kampuni, na hata ardhi anatakiwa awe na usajili na ni muhimu mamlaka na serikali zitambue uhalali wa umiliki huo, hivyo basi wewe kama msanii ili uweze kupata miliki kamili ya kazi yako na haki yako iwe na nguvu zaidi unatakiwa kusajili kazi zako.

Tukirudi kwenye kifungu cha 24 (ii) kinachosema “ 24 (2) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang'anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengineyo bila ya idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili” Kipengele hiki kinazidi kukupa nguvu na haki zaidi kama msanii kwenye kazi zako. Wewe msanii unayelalamika unaibiwa kazi zako, wewe msanii unayelalamika tatizo la urudufishaji (piracy) wa kazi za sanaa, kifungu hiki kinaeleza zaidi na kinakupa haki kisheria ya kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kukunyang’anya mali yako ambayo ndiyo kazi yako ya sanaa, hivyo basi kama uliibiwa kazi zako leo ndio mwisho, kama kazi zako zilirudufishwa leo ndio iwe mwisho, wakati umefika wa kunufaika na kazi zako, wakati umefika wa kazi yako ya sanaa kukulipa na mwisho kuujenga uchumi wa taia letu. Ili kuweza kujifunza na kujua haki zetu zaidi ningeshauri kwako msanii na vijana wenzangu kuisoma katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili tujue haki zetu na wajibu wetu kwa taifa. Kama tuliibiwa, kama tulionewa, kama tulidhurumiwa, wote kwa pamoja tuseme, IMETOSHA SASA.

MUNGU IBARIKI TANZANIA, VIONGOZI NA WANANCHI WAKE.AMINA