Jamii za kiraia: Utamaduni wa demokrasia ya kudumu

Written by Mujuni Baitani | Posted on  11 Mar 2016.

Tanzania ni nchi ambayo imekuwa na jamii za kiraia kwa lugha ya Kiingereza Civil Society, neno hili linaweza lisifahamike sana kwa wengi hapa nchini ingawa limekuwepo tangu enzi za ukoloni. Jamii za kiraia ni asasi zinazoundwa na watu kwa hiari nje ya mipaka au ulingo wa siasa za vyama kwa lengo la kutetea haki na maslahi ya umma. Katika ujumla wake kupitia vikundi vya hiari, vinaweza kueleweka ni asasi zisizo za kiserikali.


Mara nyingi jamii za kiraia hupambana kumaliza na kutokomeza matatizo katika jamii husika. Hutumia muda mwingi kuuamsha umma, kuuelimisha na kuutetea dhidi ya maovu na mapungufu yaliyopo nje ya majukwaa ya kisiasa. Jamii za kiraia zimekuwa zichukuliwa kama suluhu ya matatizo kwa wananchi tofauti. Mwanazuoni mmoja toka Chuo Kikuu cha Sheffield Uingereza Profesa David Blunkett, katika kitabu chake Renewing Democracy and Civil Society (2001) anaziita jamii za kiraia kuwa ni  “jukwaa linalounganisha raia wote wa nchi katika kuendeleza na kulinda matakwa yao nje ya ulingo wa siasa au serikali”. Pia anaendelea kwa kusema; jamii za kiraia ni mhimili wa “demokrasia, na ndiyo demokrasia yenyewe”.


Ukweli ni kwamba kushiriki pekee katika vyama vya siasa au katika kuchagua viongozi kupitia vyama vya siasa sio kigezo pekee cha kupima demokrasia nchini; kwani sio kila raia anapenda kushiriki katika mambo ya siasa; wala hatuwezi kuwalazimisha wananchi kujiunga na vyama vya siasa. Ni jambo jema kuwa hata Katiba ya nchi yenyewe kupitia Ibara 20 (1) – (4) ina ainisha wazi mipaka ya kidemokrasia na uhuru kukuza na kupigania maslahi ya umma. Pamoja na Katiba ya nchi tamko la Umoja wa Mataifa juu ya haki za raia [1948] kwamba mtu asilazimishwe kujiunga na chama cha siasa ili kumwezesha kushiriki katika kutoa maamuzi ya nchi na uongozi.


Hata hivyo kabla ya Tanzania kuingia katika mfumo wa utawala wa chama kimoja mwaka 1965, na hata kabla ya uhuru, kulikuwa na asasi zilizojumuisha Vyama vya Wafanyakazi, Vyama vya Ushirika, Vyama vya Wafanyabiashara, Wakulima wakubwa n.k. Asasi za jamii za kiraia huanzishwa kama sehemu ya demokrasia ili kuruhusu mawazo huru kutoka kwa raia wasiojihusisha na siasa kuweza kuikumbusha serikali madarakani wajibu wake kwa raia.


Tanzania ni nchi inayopambana kukua katika nyanja ya demokrasia. Ni ukweli usiopingika kwamba malumbano ya vyama vya siasa yanapoachwa kushamiri huwatupa wananchi wa kawaida nje ya mkondo wa madaraka na maamuzi muhimu ya nchi. Hivyo ni muhimu wananchi kuelewa na kusaidiana na Jamii za kiraia kubadili jamii za kitanzania.