Tupinge unyanyasaji kwa vitendo

Written by Qudrah Bernard | Posted on  11 Mar 2016.

Binadamu wote tuna haki sawa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria za kimataifa. Hata hivyo kumekuwepo na changamoto ya kukosekana kwa haki sawa katika jamii zetu, hasa kwa kinamama na watoto wa kike kunyimwa haki zao za msingi. Tanzania inajulikana kuwa ni moja ya nchi ambazo zina mikakati, mipango, na sheria nzuri lakini utekelezaji wake ndo changamoto.

Mtoto wa kike Tanzania anapata manyanyaso kutoka kila kona kuanzia ngazi ya familia, jamii, mpaka uongozi wa juu ambapo wanakosa fursa mbalimbali zinazochuliwa na mtoto wa kiume. Mwanamke ananyimwa haki zake kuanzia kwa wazazi wake, ndani ya ndoa, mpaka maeneo la kazi.

Mtoto wa kike anafanyiwa tohara bila idhini yake, kitendo ambacho kinatambulika rasmi katika baadhi ya jamii zetu. Haya mambo yanaendelea katika karne hii ya 21 na jamii wala haishangai huku serikali ikishindwa kuchukua hatua madhubuti kudhibiti hali hii. Kwenye elimu ni vile vile, binti wa kike huwa katika mazingira magumu sana ya kusoma au unyimwa kabisa fursa ya kusoma huku wakiozwa bila ridhaa yao.

Ni wakati sasa familia, jamii, na serikali kusimama kidete na kupinga kwa vitendo unyanyasaji ambao anafanyiwa mwanamke hadi sasa. Naamini tukitumia nafasi mbalimbali kama vile vyombo vya habari, sanaa, na vyombo vya dola tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi yangu Tanzania.