Je,uhuru wa kisiasa unachangia uchumi wa Taifa?

Written by Caroline Yust | Posted on  11 Mar 2016.

Je, ni kweli kwamba uhuru wa kisiasa unachangia kukua kwa uchumi wa taifa? Kuna kambi mbili kinzani zinazojitokeza kujibu swali hili. Kambi ya kwanza ni ile inayodai kwamba uhuru wa kisiasa ni sharti moja kubwa katika maendeleo ya kiuchumi; kwamba taifa huru lenye watu huru kisiasa, lina nafasi nzuri ya kupanga na kuongoza uchumi wake bila ya kuingiliwa kwa manufaa ya watu wake kuliko taifa linalotawaliwa na taifa jingine kisiasa. Kwa hili, ukweli wa usemi kwamba “siasa ni uchumi”, lakini “uchumi si siasa” unajidhihirisha wazi.

Kambi hii inaunga mkono wito wa kauli mbiu ya rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah, kwamba “Utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa, na mengine yote mtazidishiwa.”

Kambi ya pili inadai kwamba uchumi wa nchi unaweza kupangwa vizuri na kuendelea vema iwapo hautaingiliwa na siasa na wanasiasa.

Wanadai kwamba serikali lazima ijiondoe kabisa katika kupanga na kuongoza uchumi kwa kuiacha nguvu ya soko itawale; na pia kwamba uhuru wa vikundi (umma) na vyama vya wafanyakazi usiruhusiwe kuhoji mwenendo wa uchumi, soko na uzalishaji; wala kusiwe na kuhoji manufaa ya mwenendo huo kwa umma.

Kwa kambi hii, maendeleo ya “miradi” huchukua nafasi ya kwanza badala ya maendeleo ya “watu”. Mjadala huu bado ni hai na tata. Tunaambiwa tupite njia waliyopita wahenga wetu wa maendeleo ili tushikane mikono ndani ya “ufalme” wa Utandawazi. Ni njia ipi iliyo sahihi kati ya hizi mbili?.

Utata huu unaweza kuondolewa tu kwa kuangalia historia ya baadhi ya nchi zilizopitia njia hiyo ya maendeleo, lakini hata hivyo maandishi ukutani yanaonyesha si ya kutarajia.