NAKUPENDA TANZANIA

Written by Iman Rashid | Posted on  18 Mar 2016.

Maisha ya mwanadamu huanza tangu siku anapozaliwa. Biblia inasema Mungu alimtambua mwanadamu hata kabla ya kuzaliwa. Nilipozaliwa miaka zaidi ya ishirini iliyopita sikuelewa kwanini nimezaliwa – tena Tanzania, nchi ambayo imekuwa ni miongoni mwa nchi zinazoendelea: bado haijafanikiwa kimaendeleo. Nilipokuwa ninasoma sikuelewa kwanini ninasoma. Maskini mimi…! Sikuelewa.

Sikuelewa pia hali niliyokuwa ninapitia ikiwa ni pamoja na Maisha magumu, kula mlo mmoja, kukoswa ada ya shule na mengine mengi magumu, kuwa haya yote yalikuwa ni sehemu ya maisha ya watu wengi nchini Tanzania. Kuna muda nilijiuliza, mbona mimi na familia yangu tunaishi maisha haya? Wakati mwingine nikajisemea moyoni, Mbona kuna wanadamu wengine wanaishi maisha mazuri? Sio siri, niliichukia Tanzania. Nasikitika kuwa sikuwa ninaelewa. Akili yangu ilikuwa imefumbwa: imefumbwa kwa kutokutambua kuwa nilipozaliwa nilizaliwa na vipaji vya kila aina. Tena ninao uwezo wa kuibadilisha Tanzania na dunia kwa ujumla. Ingetosha tu iwapo ningeelewa mapema kuwa: akili zilizomo kichwani mwangu zinaweza kubadilisha Tanzania na hali ngumu ya maisha ya familia yangu. Lakini, ningefanya nini kipindi kile nilipokuwa sijajua vipaji vyangu. Niliishia kulalamika tu – maisha ni magumu. Upo wakati niliwalaumu viongozi wa jamii inayonizunguka na taifa kwa ujumla. Usinicheke, wengi wetu wamepitia hali hii na wengi wanaendelea kupitia kipindi hiki: wengine wanakufa wakiwa hawajua siri ya kuzaliwa Tanzania. Usiendelee tena na tabia hii: acha mara moja kulalamika, umiza kichwa chako kuyatafuta majibu ya matatizo yanayojitokeza.

Ilikuwa ni siku ile nilipotambua kuwa Tanzania imeniwekea kila aina ya fursa na kinachotakiwa ni mimi kutoka na kuzitafuta nikitumia uwezo wa kuzungumza nilionao na kuwafundisha wanadamu wengine. Nilijifunza kutoka na kuanza kuzitafuta fursa. Sikuangalia tena nimesomea nini bali nilijiuliza ninaweza kufanya kitu gani na nilipoyapata majibu nikaamua kuanza kutumikia kile ninachoamini ni kipaji changu: kipaji cha kufundisha watu wengine lakini si kwa kukaa darasani nikiwafundisha. Ninaamini hiki ndicho ninachoweza kufanya na hivyo nilianza na ninaendelea kufanya hivyo. Sikuelewa ninachokifanya lakini kumbe ndio nilikuwa ninashiriki maendeleo ya jamii yangu. Nikiendelea na zoezi hili la kufundisha ndipo nilipobaini kuwa Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kila aina ya Baraka. Pia, Baraka zinajidhihirisha pale unapoanza kutumia kipaji chako kwa ajili ya jamii yako. Niliamini na ninaendelea kuamini pesa si lolote bali jamii kwanza inufaike na jamii yangu kisha pesa zitakuja kama sehemu ya pongezi, shukrani na Baraka zitokazo kwa Mungu.

Nimejifunza kuipenda jamii yangu ambayo watu wengi bado wako na mtazamo kama niliokuwa nao miaka mingi. Ninatamaa ya kuona watu wanabadilika na kuanza kutumia karama zilizo ndani yao kuyafikia maisha ya mafanikio. Nimejifunza kuwa Tanzania ni nchi ambayo sipo kwa bahati mbaya – Nakupenda Tanzania uliyejaa kila aina ya fursa, utajiri, mali na kila aina ya mambo mema kwa ajili ya maisha yangu.