NUSU NUSU

Written by Eberhard Osward | Posted on  18 Mar 2016.

Kuna msemo mmoja wa wahenga unaosema eti “Nyundo inayotumika kujengea mara nyngi ndio hiyo hiyo itumikayo kubomolea”,  kwa muda mrefu nilikuwa sijapata kuelewa maana ya msemo huo. Ila baada ya kutafakari kwa kina hasa kwa kuitazama sanaa yetu, nimekuja kupata maana. Siku zote nimekuwa nikiitazama sanaa yetu Tanzania kwa jicho la ukaribu sana, nimejaribu kujifunza vitu vingi sana kwenye sanaa lakini kikubwa zaidi nilichokuja kugundua ni kwamba sanaa ni kama nyundo, ina upande mmoja wa kupigilia msumali na upande mmoja wa kung’olea msumari. Hapa namaanisha sanaa hii imekuwa msingi wa kujenga jamii bora kwa kiasi chake na sanaa hii pia imekuwa kifaa cha kubomoa jamii, maadili na hata utamaduni wetu kwa ujumla.

Nakumbuka kipindi nipo shule ya msingi, nilikuwa napenda sana muziki, moja kati ya nyimbo za kipindi kile kama Starehe ya Ferooz,Darubini Kali ya Afande Sele,jukumu letu ya Prof. Jay akishirikiana na Mwana Falsafa, zilikuwa ni nyimbo zilizobeba ujumbe na maadili makubwa sana, wasanii waliuenzi utamaduni mfano mkubwa Saida karoli, Wane Star ambao walitumia lugha zao za asili, mavazi ya asili, msanii kama Mr. Ebbo Mungu amlaze mahali pema peponi, yeye alitumia sanaa kuuelezea umasai. Lakini nikija kuangalia sanaa yetu kwa sasa imekua sana, wasanii wanafaidika sana, lakini Swali kwako wewe  unayesoma makala hii.

Je, sanaa hii ya sasa inauenzi utamaduni?. Je, Unafikiri sanaa hii inajenga kizazi bora? Maana mimi naona kama vile watoto wengi siku izi wanaharibika sitaki kusema ni sababu ya sanaa ila nitadiriki kusema sanaa ina nafasi yake katika hili, nikiangalia mavazi, yamekosa maadili kwenye nyimbo ya Where is Love Ya Black Eyes Peas wanasema watoto wanataka kuigiza maisha wanayoyaona kwenye Tv na hapa ndio ninaloliona Tanzania, watoto wanapoteza maadili kuanzia mavazi na sehemu kubwa ya maisha yao.

Nitamaliza kwa kutoa wito na ombi kwa wasanii, ni kweli mnapata ela, mnaendesha maisha, lakini pia ningependa mjiulize swali moja, Je,Mnataka Tanzania hii iwe ya namna gani, mnawezaje kutumia sanaa yenu kuleta maendeleo ya utamaduni, maadili, uchumi na siasa?. Bado naamini sana katika sanaa na uwezo wake wa kuubeba utamaduni wetu kimataifa.