Tanzania Ndio Mimi, kwenye Tanzania Mpya

Written by Eberhard Osward | Posted on  18 Mar 2016.

Moja kati ya hadhina kubwa tuliyojaliwa nayo binadamu ni vipaji. Bila kuona aibu nadiriki kusema kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi ambayo imebarikiwa kuwa na vijana wenye vipaji sana. Swali linakuja Je, Tunatumiaje vipaji hivi kujenga jamii bora na nchi yetu kwa ujumla?. Ukijaribu kufuatilia kwa umakini utagundua kuwa asilimia kubwa ya vijana nchini wanatumia vipaji vyao hasa sanaa na michezo katika kujiajiri na kuweza kuendesha maisha yao.Bado nafikiri na naamini kuwa vipaji hivyo bado vinaweza kufanya makubwa zaidi hasa kwenye kuleta uongozi bora ambao ndio msingi wa maendeleo. Katika makala hii nitajaribu kuiangalia sanaa na jinsi inavyoweza kusaidia katika kuleta maendeleo Nitaelezea mada hii  kwa kutumia nyimbo mbili ambazo ni Tanzania ndio Mimi iliyoimbwa na Tanzania Bora Artists na Tanzania Mpya iliyoimbwa na We Belong To Art.

Nitaanza na Tanzania Mpya ya We Belong To Art, Binafsi nikiwa kama kijana na miongoni mwa watu walioshiriki kuiandaa na kuisimamia nyimbo hiyo, lengo kuu lilikuwa ni kufikisha ujumbe kwa jamii yetu, ilikuwa ni kuleta mtazamo chanya ambao kwa asilimia kubwa sanaa ya nchi yetu imekuwa ikisahau, fuata link hii kuuangalia https://www.youtube.com/watch?v=Sul-wbZnWPg

Tanzania ndio mimi, mimi na wewe tuishi kwa pamoja, ni moja kati ya mstari unaonivutia kwenye nyimbo hii ya Tanzania ndio mimi ya Tanzania Bora Artists, nyimbo ambayo imesheheni mashairi mazuri yenye kuvuta hisia na kuzungumzia uzalendo, ndani ya nyimbo hii kuna mengi yameimbwa ikiwa kama “Kama kazi nitafanya, pigania uchumi simama” akiwa na maana sanaa inaweza jenga uchumi, pia mstari kama “Nyeusi ni sisi wazalendo” ikizungumzia uzalendo, angalia link hii hapa     https://www.youtube.com/watch?v=0T_gAkeoQ4c kusikiliza nyimbo hiyo.

Baada ya kuangalia kazi hizo mbili zitokanazo na vipaji katika sanaa utaamini kuwa sanaa ina nguvu ya kuleta mapinduzi katika maisha yetu, sanaa na vipaji ni zaidi ya burudani bali ni maisha yetu ya kila siku.