Kwanini Umasikini?

Written by Qudrah Bernard | Posted on  25 March, 2016.

Kama ni mali asili zipo kibao, kama ni madini yapo kibao, mpaka tunawapa wageni kwa kiwango kidogo sawa na bure, kama ni maziwa yapo kibao , kama ni ardhi iko kubwa jamani na bado hadi sasa Tanzania ipo katika nchi zinazoongoza kwa umasikini barani Africa na duniani. Nashindwa kuelewa hivi ni kwanini umasikini unazidi kuenea katika nchi yetu pamoja na vyote tulivyo navyo.

Maeneo ya vijijini mkulima anaamka kabla jogoo hajawika ili tu awahi shambani . kila siku mvua yake jua lake ili mradi tu apate kitu kidogo, ili mkono uende kinywani . Upo mtizamo kwamba sababu ya kuendelea kwa umasikini wetu ni kwa kuwa watanzania tunamiliki mali lakini hazina urasmi yamkini ya kutuwezesha kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kiserikali ,na ndio maana ukaja mkakati wa kurasimisha mali hizo kama harakati mojawapo ya kupambana na ufukara nchini kupitia mikopo hiyo

Katika harakati za kusaidia kuondokana na umaskini tumehimizwa kuifuata fursa yoyote inapotokea mfano  kununua hisa katika mashirika tofauti nchini swali ni je mwananchi anayeishi kijijini ana elimu gani kuhusu swala zima la hisa? Umasikini umeendelea kuenea nchini kwetu katika sekta mbalimbali. Tatizo jingine ni ukosefu wa ajira kwa vijana  wengi nchini ila kimantiki hili halikupaswa kuwepo kutokana na sayansi na teknolojia kuenea ambapo matumizi ya maarifa yameongezeka na pia kumekuwa na urahisishwaji wa kazi mbalimbali tofauti na kipindi cha analojia. Hivyo inawezekana kuwa tatizo sio ajira ila tatizo ni vijana wengi nchini hawana elimu .

Kuna sekta kama kilimo lakini vijana wengi wanaikimbia na kusema kuwa wazee ndio wanapaswa kufanya kazi za kilimo ,pia tumeona serikalini ufisadi na wizi umetawala kile ambacho walipaswa kupewa wananchi kwa manufaa yao wenyewe kinachukuliwa na watu walioko na madaraka. Hiyo inapelekea watu na nchi kuendelea kuwa masikini.

Umefikia wakati sasa tujishughulishe ili kuondoa na kumaliza umasikini nchini, tuwashughulikie wezi wote mafisadi na hata wale waomba rushwa katika sekta mbalimbali mfano sekta ya afya sekta ya kilimo, sekta ya elimu,miundombinu  na usafiri  nk ili tuweze kulinusuru taifa kutokana na umasikini. Pia vijana wafanye kazi kwa bidii na kutumia rasilimali tulizonazo ili tuweze kuliletea mapato taifa letu na wananchi kwa ujumla.