Hauishi Kunishangaza

Written by Imani Rashid | Posted on  8 April, 2016.

Sikumbuki sana ila ninaukumbuka upendo wako tangu kutungwa kwa mimba yangu. Kuna wakati ulisema na mimi, ukaniambia nitulie hukohuko tumboni nisijigeuzegeuze, nikatulia. Hukujua kama nitakuwa wa jinsia ya kike au kiume, lakini ulijifunza kunipenda. Nilikupelekesha hata ukaanza kubaguabagua vyakula, watu wa kukaa nao na wakati mwingine kuwachukia baadhi ya watu wengine: lakini hukujali bali uliendelea kunivumilia. Siku nazaliwa ulitokwa na damu nyingi sana! Hukuchoka kuvumilia. Nilipozaliwa ulinikumbatia kwa upendo mkubwa hata nikakujua na muda uleule nikaufundisha mdomo, moyo na akili yangu yote kuwa wewe ndio mama. Tena ukaendelea kunilea kwa upendo ule ule huku ukinifundisha yapi ni mema na yapi ni maovu.

Sikumbuki sana, lakini nilipoanza kuelewa kinachoendelea duniani, nikabaini kuwa wewe ndio jinsia isiyopewa kipaumbele, inayozalisha lakini mwanaume ndiye anatumia faida, unayelea lakini nikikosea mimi matusi yote yanaelekezwa kwako. Sikuelewa kwanini unanyimwa nafasi ya kuongoza kwenye jamii hadi serikali ikaanza kidogo kidogo kukutengea asilimia 30% kwenye nafasi za bunge la nchi yangu. Nilipokuwa shule nikatambua kuwa kumbe hata hizo zilikuwa ni harakati zako binafsi na angalau mwaka 1992 katika mkutano wa Beijing ukapiga hatua kwa kujikomboa, japo kidogo. Zaidi sana katika nchi yangu nikaambiwa kilimo ndicho angalau kwa asilimia 75 kinachangia uchumi wa taifa. Halafu nikafikiria kuwa anayeshinda shambani akilima, anayemwagilia mazao, anayepanda mbegu ni wewe. Nilipozitazama hospitali ulikonizaa nikaona unakufa kwa kukoswa huduma. Wakati mwingine unatokwa na damu nyingi sana kupita kiasi, tena wakati mwingine hata mtoto unayemzaa anaweza kufariki muda mfupi mara baada ya kujifungua kutokana na ukosekanaji wa huduma. Nakumbuka nilijisemea mwenyewe moyoni, “huyu ndiye anayeongoza kwa kuchangia pato la uchumi wa nchi yangu, bado kuna wanaume ndio wanaompangia, tena kwa kiasi kidogo tu jinsi ya kupata huduma. Tena hawajali hata watoto unaojifungua, wamekuweka pembeni kweli kweli! Ukatili ulioje.

Mwaka 2016 nikakusikia unasema “50-50 ifika 2030: tuongeze jitihada” nikatafakari tena, “kwanini hauthaminiwi? Kwanini unabezwa? Kwanini uko nyuma ya mwanaume?” Moyo wangu ukaumia sana, nikamua nikuandikie waraka huu ukukumbushe kuwa, wewe ni wathamani sana katika dunia hii. Hakuna chochote ambacho kinakushinda mwanamke kufanya. Unao ushawishi, mimi ni shabiki wako. Niambie mimi mwanao tu, nijifunze kukupenda na kukuheshimu ili siku nikikua, nikujengee hospitali nzuri, pia nimjali mtoto utakayemzaa. Wewe ndio mama wa ulimwengu, bila wewe mimi nisingekuwepo. Bila wewe nisingeweza kuziishi ndoto za maisha yangu, kadhalika, nisingesoma hata shule. Roho yangu inanikumbusha, niiambie dunia yote juu ya wema wako, halafu niiombe iunge mkono jitihada zako pia iijali afya yako. Isijisahau kamwe kuwa bila wewe hakika wanadamu wasingekuwepo hapa duniani na kufikia idadi ya bilioni 7.1