Usalama Barabarani

Written by Leyla Mchawe | Posted on  8 April, 2016.

Kuna matatizo mengi nchini Tanzania ambayo huwezi kuyasikia kwenye redio, huwezi kuyaona kwa televisheni, huwezi kuona bendera imeshushwa nusu mlingoti kwa ajili yake, huwezi kuona wacheza mpira wamevaa vitambaa mkononi kuashiria janga. Lakini ni majanga makubwa na yanahitaji kutambuliwa na kila mtu.

Hivi unafahamu ya kwamba kila mwaka karibuni watu 1.25 millioni hufariki kwa ajali za barabarani duniani? Hii inaweza kuonekana ni idadi ndogo, lakini hebu tujiulize ni ndugu zetu wangapi wamevunjika miguu au mikono kwasababu ya ajali za pikipiki au magari? Wangapi wamefariki kwa ajili ya ajali za barabarani? Je ni nguvu kazi ngapi za taifa zimepotea kwasababu ya ajali? Ripoti nyingi duniani zinaonyesha kati ya watu 20-50 millioni wanapata ajali sizizo na maafa makubwa, japokuwa wengi wao huishia kupata ukilema.

Chakushanganza zaidi ajali za barabarani ni chanzo cha nane duniani katika vyanzo vya vifo yaani lina kasi ya kuua kama UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu. Vilevile tisa kati ya vifo kumi vitokanavyo na ajali za barabarani hutokea Afrika. Nchini Tanzania ajali za barabarani miaka ya hivi karibuni imezidi wakati wenzetu nchi nyingine wakujaribu kupunguza. Kwa bahati nzuri, katika maeneo kama vile Marekani na Ulaya, vifo vya barabarani vimekuwa vikupungua kwa kasi. Mafanikio haya yamepatikana na jitihada ambazo nchi hizo hufanya katika kuzuia ajali za barabarani. Wameweza kushughulikia mambo kama mwendokasi, kuendesha gari huku dereva akiwa amelewa, kuvaa helmeti, mikanda ya usalama na vizuizi kama matuta na zebra barabrani. Lakini tunajua pia kwamba nchi hizi kuwa na mifumo ya dharura (911) ya kutibu waathirika wa ajali za barabarani, ambayo huweza kuokoa maisha na kupunguza ukali wa majeruhi, kuepusha maisha ya ulemavu.

Bila shaka, mengi zaidi yanatakiwa yafanyike nchini kwetu ili kuzuia ajali za barabarani ambazo zinatishia maisha yetu. Nakumbuka niliwahi kufanya utafiti japokuwa nilipata majibu machache ya hasara kamili itokanayo na ajali, lakini utafiti uliofanyika mwaka 2010 uliripoti kwamba ajali za barabarani zinasababisha hasara ya 3% ya pato la taifa duniani na kwa Tanzania ni asilimia 5%. Kwa miaka mingi ajali za barabarani zilikuwa hazijawekewa maanani lakini kwenye agenda ya dunia ya mwaka 2025 wameweka agenda ya kupunguza ajali ifikapo mwaka 2020. Lakini kwa jinsi hali ilivyo sasa nchini Tanzania hii kitu itakuwa ngumu sana kufikiwa.

Hali ni mbaya jamani! Naomba serikali yetu ijaribu kuweka namba za dharura ambazo watu wanaweza kupiga endapo ajali zikitokea, hii itasaidia kupunguza idadi ya vifo kwa majeruhi. Lakini pia wananchi inabidi tuzinduke, tusipande pikipiki bila kuvaa helmeti, pia dereva akiendesha kwa mwendo kasi tushuke , tusisubiri hadi ajali imetokea ndio tuseme dereva alikuwa anaendesha kwa spidi. Na wananchi tuache kuendesha magari machakavu.