MASHAIRI YA MAKILLA: Afya yako ni deni

Written by Mujuni Baitani | Posted on  8 April, 2016.

AFYA ukijaliwa, hilo ni deni tambua,
Yafaa kuitumia, kwa yale yatayokufaa,
Siku zikishatimia, thawabu kujivunia,
Afya yako ni deni!
 
Naam utashangaa, haya ukiyasikia,
Bali nakuhakikishia, ni ukweli ulotimia,
Kama hukuyajua, macho nimekufungua,
Afya yako ni deni!
 
Ni deni ninakwambia, utakuja kudaiwa,
Muumba unayemjua, budi kuliulizia,
Nawe kumsimulia, jinsi ilivyokuwa,
Afya yako ni deni!
 
Askari hudaiwa, na wao pia raia,
Ole wao watumiwa, na hawatasaidiwa,
Kila wakisingizia, kidole kwa hurejea,
Afya yako ni deni!
 
Nguvu waliotumia, wanafunzi kuwavaa,
Au wapole raia, waliojikutania,
Na maandamano yakawa, salama yenye ulua,
Afya yako ni deni!
 
Husimulia jamaa, kisha kuhukumiwa,
Afya waliitumia, vibaya isivyofaa,
Motoni wataingia, huku wakijijutia,
Afya yako ni deni!
 
Nesi wanaowaua, wagonjwa huku wajua,
Nao watasimulia, huku ukiwa wakiwa,
Wasiamini kujua, wenye aya wayajua,
Afya yako ni deni!
 
Madaktari nao pia, kitabu kitasogea,
Ukweli kuugundua, sivyo walivyoamua,
Nafsi kutangulia, Muumba hakukusudia,
Afya yako ni deni!
 
Wanasiasa wakiwa, zamu itawafikiya,
Midomo itanyamaa, la kujibu kutojua,
Midomo itaamua, yenyewe kujisemea,
Afya yako ni deni!
 
Afya waliyopewa, wenyewe walitumia,
Kingi wakajimegea, chakula kilichokuwa,
Dhuluma wakaamua, vya watu kuvichukua,
Afya yako ni deni!