Aboubacary aka Abou

Written by Leyla Mchawe | Posted on  15 April, 2016.

Abubakary au kama wenzie hupenda kumuita abou ni mtoto wamiaka saba anaependa sana kusoma. Anatokea katika Wilaya ya pangani kijiji cha madanga. Kijiji madanga shule za msingi ni chache na hazina vifaa na hadhi zakuwa shule imefikia hatua viwanja vya kufanyia mazoezi vinabadirishwa kuwa madarasa. Abou anakosa rasilimali muhimu kwa ajili ya kupanua mawazo yake yatakayoweza kuporomoa na kuvunja kuta za umasikini zinazomzunguka.


Duh! Chakushanganza nikua walimu mkoani Tanga kila siku wanalalamika kuwa hawalipwi mshahara wakutosha kukidhi mahitaji yao wala mahitaji ya shule, hali ni tofauti na shule za kulipia ambazo walimu hulipwa vizuri na hata hadhi ya shule ni zakuridhisha. Chakusikitisha ni kwamba familia zenye uwezo mdogo hazina jinsi zaidi ya kuwapeleka watoto shule za serikali ambazo hali yake ni yakusikitisha. Ni wazi kuwa, bajeti ya shule za serikali na sera ya elimu inabidi kufanyiwa marekebisho. Haiwezekani kuwa eneo aishio mtu na kipato cha wazazi wake kiwe kipimio cha ubora wa elimu kwa watoto. Kila mtu anahaki ya kupata elimu bora, kama ibara ya 11 ya katiba ya mwaka 1977 inavyosema. Shule nyingi za msingi za serikali zinatoa bora elimu na sio elimu bora, na familia nyingi za kimasikini zinalazimika kuwapeleka watoto wao kupata bora elimu kwasababu hawana uwezo wakuwasomesha katika shule zenye elimu bora.

 

Hebu tujiulize Abou atafanikiwa kuondokana na umasikini? Je ataweza kuwasaidia wazazi wakizeeka ya hali kuwa yeye mwenyewe hakupata elimu bora?. Nini kifanyike ili matabaka kwenye elimu yaishe?. Naamini serikali lazima ihakikishe pesa zinazotengwa kwaajili ya  marekebisho ya shule na mishahara ya elimu zitumike kama ilivyopangwa ili kusaidi wanafunzi kupata elimu bora. Muhimu zaidi, fedha zielekezwe kwenye ujenzi wa shule na manunuzi ya madawati na chaki ili elimu iweze kupatikana kwa ukaribu na ufanisi zaidi.